Loading...
Home Habari Je kushinda njaa ni njia sahihi na salama kiafya kupunguza mwili?

Je kushinda njaa ni njia sahihi na salama kiafya kupunguza mwili?

196
SHARE

Kuna njia nyingi za kupunguza mwili ambazo hutangazwa kwenye televisheni na mitandao ya kijamii. Lakini njia salama na inayopigiwa chapuo na wataalamu wa afya ni kufanya mazoezi ya viungo na kubadili mfumo wa chakula kwa kuanza na mlo sahihi.

Katika kubadili mpangilio wa kula kuna mambo mengi, kwani kuna elimu mbali mbali zisizo rasmi zinatolewa katika mitandao juu ya kupangilia chakula. Hata hivyo kwa mujibu wa mitandao mtu anaweza kupungua haraka endapo atafuata mlo anao elekezwa.

Kuna mpangilio wa chakula wa siku 7, siku 10 na mpaka siku 21. Na mtu anaweza pungua kuanzia kila 3 mpaka 15 inategemea kama atafuata kwa umakini.

Supu ya kabeji, mlo wa kijeshi ama kwa kingereza ‘Military Diet’, na mlo wa yai ama ‘Egg diet’ hizi ni baadhi tu ya njia za haraka za mpangilio wa chakula au diet ili kupunguza unene kwa haraka zaidi.

Je walio tumia wamesaidika? BBC imeangazia safari ya kupunguza uzito ya Linda mama wa mtoto mmoja na muuguzi nchini Tanzania anasema huwa anapungua na kuongezeka.

“Nina mwili mkubwa sana na siuifurahii hata kidogo, natamani nipungue sana, nimejaribu hizi diet za kupungua haraka kwa miaka kama minne sasa sema ndio hivyo, napungua halafu nanenepa tena. Mfano mwezi wa tisa nilikuwa na shughuli nkajipunguza yaani nakuwa nakula mlo mmoja tu sema nlipoacha tu nkaongezeka mpaka aibu,” Linda anaiambia BBC

Hata hivyo mama huyu anaamini kuwa mwili wake ni wa kurithi kwani ndugu zake wengi ni wanene hivyo kupungua kwake si kazi rahisi.

“Mie mwili wangu hauwezi kupungua kirahisi maana wazazi wangu pia wanene sana na mi mwenyewe naelewa hilo. Kwa sababu nishafanya sana hizi diet na ndo kwanza nimeambulia vidonda vya tumbo. Hivyo naamini ni mambo ya kijenetiki ntapungua tu wakati ukifika.” Linda anaongeza.

Je njia hizi ni salama?

BBC imezungumza na Daktari wa magonjwa ya binadamu aliyejikita kwenye magonjwa ya lishe na mwandishi wa vitabu vya afya ya jamii maarufu kama sayansi ya mapishi nchini Tanzania Dkt. Boaz Mkumbo ambaye amebainisha kuwa kutojua njia sahihi kunawafanya wengi wanaangukia katika njia ya kujinyima kula lakini ni hatari kwa afya.

“Si watu wote wanaweza kujinyima chakula, daktari anaweza kumzuia mtu kula lakini hawezi kuizuia njaa. Njaa sio tendo la hiari, hivyo kujinyima sana huleta udumavu wa mwili mtu unachakaa kwa sababu ya kukosa viini lishe,” anasema dokta Boaz.

Madhara ya kujinyima kula:

  • Kukosa viini lishe katika mwili, hali inayopelekea kudumaa na uchakavu wa mwili yaani nuru kupotea kisha kuwa kama mgonjwa.
  • Si watu wote wanaweza kujinyima kula kwasababu huwezi kuizuia njaa.
  • Unaweza kupata hatari ya kushuka kwa sukari gafla au presha ikashuka gafla kwasababu yakukosa viini lishe muhimu
  • Si watu wote wanaweza kudhibiti uzito ubaki pale pale hata baada ya kupungua kwani si njia endelevu, huwezi jinyima maisha.

Hata hivyo daktari huyo amepinga vikali tabia ya watu kujinyima kula kwani haina matokeo ya kudumu, sababu unapoacha kujinyima mwili utaongezeka.

“Kujinyima kula ili kupunguza uzito si njia endelevu, huwezi jinyima milele. Njia nzuri ya kupungua uzito ni kuzingatia ubora wa chakula. Katika sayansi ya mapishi tunaamini kila chakula ambacho tunakiweka mwilini kina muitikio tofauti. Mwili ukiupa sukari na vyakula vya wanga unamimina homoni nyingi za kunenepesha. Lakini nikakupa mayai, samaki parachichi na baadhi ya matunda ambayo yana sukari kidogo kama matango mwili utaitikia kwa kumwaga homoni ya kunenepesha kwa kiwango kidogo sana. Utapata virutubisho vyote na mwili hauta fubaa wala kusinyaa,” Dokta Boaz ameiambia BBC

Hata hivyo daktari Boaz ameenda mbali zaidi na kufafanua kuwa mtu kuwa na tumbo kubwa ama kitambi si ulafi.

“Kitambi hakisababishwi na ulafi wala uvivu, ukimwambia mtu ni ulafi atajinyima kula ukisema uvivu atafanya mazoezi lakini hatoangalia ubora wa anachokula. Sikuizi nashangaa sana sehemu za mazoezi unakuta mtu ametoka humo anafika nje anaanza kunywa soda. Bila kujua mwili wake unaenda kumwaga homoni nyingi za kunenepesha. Kitambi husababishwa na homoni, ili kudhibiti kitambi na mlipuko mkubwa wa magonjwa ya lishe lazima tuzingatie ubora wa chakula ili tuweze kufikia malengo yetu ya afya na kuepuka homoni za unene kumwagika,” dokta boaz anaiambia BBC.

Hata hivyo daktari huyo amefafanua kuwa vyakula vya wanga, juisi za viwandani na soda ni baadhi tu ya vyakula ambavyo hupelekea kumwagika kwa homoni za unene kwa wingi.

Makala na BBC SWAHIL

Facebook Comments