Loading...
Home Habari Felix Tshisekedi: Mgombea wa upinzani ashinda uchaguzi wa urais DRC

Felix Tshisekedi: Mgombea wa upinzani ashinda uchaguzi wa urais DRC

110
SHARE

Felix Tshisekedi ameshinda uchaguzi wa urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tume ya uchaguzi imesema.

Matokeo ya awali yanaonyesha mgombea huyo wa upinzani amemshinda mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu, pamoja na mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na serikali Emmanuel Shadary.

Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni) Corneille Nangaa, alisema mapema Alhamisi kwamba Bw Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na “anatangazwa mshindi wa urais mteuleW

Tshisekedi alipata zaidi ya kura 7 milioni naye Bw Fayulu akapata kura takriban 6.4 milioni, huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akipata takriban kura 4.4 milioni.

Matokeo yaliyotangazwa na CENI:

  • Felix Tshisekedi 7,051,013 (38.57%)
  • Martin Fayulu Madidi 6,366,732 (34.83%)
  • Emmanuel Shadary 4,357,359 (23.84%)

*Waliojitokeza kupiga kura kwa mujibu wa CENI ni 47.56%.

Bw Fayulu ameyapinga matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.

Ameambia Idhaa ya Kifaransa ya BBC kuwa: “Hii ni kashfa mbaya sana. Matokeo haya hayana uhusiano hata kidogo na ukweli halisi. Raia wa Congo hawataukubali utapeli kama huu daima. Felix Tshisekedi hakupata kura 7 milioni, haiwezekani. Alizitoa wapi?”

Tamko la Ufaransa na Ubelgiji

Barnabe Kikaya Bin Karubi, ambaye ni mmoja wa washauri wakuu wa Rais Joseph Kabila amekubali matokeo hayo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Amesema: “Bila shaka hatujafurahia kwamba mgombea wetu alishindwa, lakini raia wa Congo wameamua na demokrasia imeshinda.”

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters ameomba kuwepo na ufafanuzi kuhusu matokeo hayo akisema ushindi wa Bw Tshisekedi unaenda kinyume na uhalisia mashinani.

“Kanisa Katoliki la Congo lilifanya hesabu yake na kutoa matokeo tofauti kabisa,” amenukuliwa na shirika hilo.

Nchi ya Ubelgiji ambayo iliitawala DRC wakati wa ukoloni imeungana na Ufaransa katika kutilia mashaka matokeo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje Didier Reynders amenukuliwa la shirika la habari la Reuters akiiambia redio ya taifa RTBF kuwa Ubelgiji itatumia nafasi yake ya muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka taarifa rasmi ya kilichotokea.

“Tuna mashaka na inabidi tuhakikishe na kujadiliana suala hili katika vikao vya Baraza la Usalama,” Bw Reynders ameongeza.

Tamko la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa wadau wote kujiepusha na vurugu.

“…waelekeze mizozo yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi kwa mifumo na taasisi zilizopo kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, msemaji wake Stephane Dujarric, amesema akiwa mjini New York.

Umoja wa Afrika (AU) wametaka mzozo wowote kuhusu matokeo ya uchaguzi huo yatatulie kwa njia ya amani.

Mkuu wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat amesema: “Ni muhimu kwa mtanziko wowote wa matokeo, hususani kuwa hayajaakisi matakwa ya wananchi, inabidi utatuliwe kwa njia ya amani kwa kutumia sheria na makubaliano ya kisiasa kwa pande zinazohusika.”

Iwapo matokeo hayo yatathibitishwa, Bw Tshisekedi atakuwa mgombea wa kwanza kabisa wa upinzani kushinda uchaguzi wa urais tangu DRC ilipojipatia uhuru.

Bw Tshisekedi yuko kwenye muungano wa kisiasa aliyekuwa mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe UNC ambapo walikuwa wamekubaliana kwamba Tshiskedi atagombea wadhifa wa rais naye Kamerhe awe waziri mkuu iwapo muungano wao utashinda urais.

Rais Joseph Kabila anatarajiwa kuondoka madarakani baada ya kuongoza kwa miaka 18.

Mgombea wake aliyemteua kuwakilisha muungano tawala Emmanuel Ramazani Shadary amemaliza wa tatu.

Martin Fayulu ambaye awali alikuwa mgombea wa pamoja wa muungano wa upinzani kabla ya Tshisekedi na mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe kujiondoa kutoka kwenye muungano huo na kuunda muungano wao wawili, alimaliza akiwa nafasi ya pili.

Facebook Comments