Loading...
Home Habari Zitto Kabwe Aitupia Lawama Serikali Kushuka Kwa Bei Ya Korosho Mwaka Huu

Zitto Kabwe Aitupia Lawama Serikali Kushuka Kwa Bei Ya Korosho Mwaka Huu

148
SHARE
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Serikali haipaswi kukwepa lawama kwenye suala la uuzaji wa korosho na ikubali kuwa imefanya makosa.
Zitto ametoa kauli hiyo leo Oktoba 28, 2018  zikiwa ni siku chache baada ya Serikali kusitisha minada ya zao hilo mpaka Oktoba 30 itakapotoa maelekezo mapya baada ya wakulima kugoma kuuza korosho zao kutokana na bei ndogo waliyotaka wanunuzi.
“Badala ya Serikali kulichukulia zao la korosho kama la kimkakati imekuwa haisikii, haielewi, na sasa imeharibu kuku anayetaga mayai ya dhahabu katika nchi yetu,” amesema.
Amesema korosho ndio zao pekee la kuiokoa nchi kwamba Serikali ilieleza kuwa imepata wanunuzi wa korosho kutoka Marekani watakaonunua kilo moja kwa Sh5,000 jambo ambalo si kweli.
Pamoja na ahadi hiyo ya Serikali, Zitto amesema kufuatia taarifa alizonazo kutoka Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na wanunuzi, uzalishaji wa zao hilo utashuka kwa asilimia 40.
“Mnaweza kuona fedha za kigeni tunazoenda kupoteza kwa uamuzi wa Serikali kuchukua fedha zote za export levy (ushuru wa forodha) badala ya kupeleka zinakostahili,” amesema Zitto.
Kuhusu kushuka kwa uzalishaji na bei, amesema kutaathiri  mapato ya wakulima na Serikali pia.
Msimu wa mwaka jana, wakulima waliuza kilo moja kwa Sh4,000 hivyo kuiwezesha Serikali kuingiza Dola 209 milioni za Marekani.
Minada mitatu ya kwanza iliyoandaliwa na Chama cha Ushirika Tandahimba na Newala (Tanecu), Masasi na Mtwara (Mamcu) na Ruangwa, Nachingwea na Liwale (Runali) haikufanikisha mauzo ya tani 5,100 kutokana na kushuka kwa bei.
Bei kubwa zaidi kwa kilo moja kwenye mnada wa Tanecu uliohudhuriwa na kampuni 15 ilikuwa Sh2,717 na Sh2,520 kwa Mamcu kulikokuwa na kampuni nane wakati ni kampuni tano pekee zilijitokeza mnada wa Runali ambako bei ilikuwa Sh2,657.
Kutokana na mwenendo usioridhisha wa mauzo ya korosho mwaka huu, wiki iliyopita, Rais John Magufuli aliagiza kuondolewa kwa kaimu mkurugenzi wa CBT, Profesa Wakuru Magigi.

Facebook Comments