Loading...
Home Habari Mufunje: Daraja hatari linaloviunganisha vijiji viwili Kenya

Mufunje: Daraja hatari linaloviunganisha vijiji viwili Kenya

178
SHARE

Daraja la Mufunje ni eneo maarufu mno kwa wenyeji wa eneo la Nzoia magharibi mwa Kenya.

Daraja hilo ambalo limejengwa kwa nyaya pamoja na mbao na linaviunganisha vijiji viwili, wale wanaoishi upande wa Nzoia na wale walioko upande wa Bukoba.

Jina Mufunje lina maana ya kufunganisha kitu pamoja, maana inayo endana sawa na muonekano wa daraja lenyewe.

Limeunganishwa tu kwa nyaya, mfano wa zile ambazo hutumika kusambaza nguvu za umeme pamoja na mbao na kamba.

 

Lakini kwa macho ya mgeni, moja kwa moja hisia ya hatari hukujia unapolitazama daraja hilo.

Ni kivukio kikuu kwa wakaazi wa eneo hilo, wazee kwa vijana wanaoonekana wakivuka pasi kuhisi hatari ya mto unaopita chini ya daraja hilo ulio na wanyama hatari kama mamba.

Mwandishi wa BBC Anne Ngugi aliyefika katika eneo hilo anasema, kila mtu analenga safari yake kuvuka hadi ng’ambo nyengine.

Na ni hapa ambapo pia alishuhudia mama mmoja kwa jina Metrin Midinyo akiwa na mtoto wake mngongoni akivuka.

Metrin anasema kuwa yeye haogopi wala hana wasiwasi wowote wa kuvuka daraja hili , japo anakubali kuwa mara kwa mara nyaya za daraja hili huoza na kukatika.

Anaeleza kwamba pia mbao zenyewe huoza na hutokea mtu huenda akajipata ameanguka katika mto Nzoia unaopita chini, mojawapo ya mito mikubwa nchini Kenya.

Patrick Wekesa ana miaka 25 anaeleza kuwa tangu utotoni mwake akikumbuka mwaka wa 1995 yeye pamoja na watu wa jamii yake walikuwa wanatumia daraja hilo.

Yeye ni fundi wa mbao , kila siku yeye huvusha mbao kupitia daraja hilo la Mufunje kutoka upande mmoja hadi mwengine.

Sio hayo tu, anasema kuwa yeye hawezi kumudu kupita njia mbadala ambayo humgharimu takriban dola karibu 5 kupita njia nyingine ambayo ni ndefu mno.

Daraja hili la Mufunje linaunganisha vijiji ambavyo vinahitajiana mno.

Upande mmoja kuna shule na hospitali , na upande mwengine kuna soko na maeneo mengine ya kibiashara.

Kwa hivyo licha ya hatari iliyoko kwenye daraja hili wenyeji wwamezoea kuwa ikiwa litakatika wanaungana tena kulikarabati.

Moses Werunga mkaazi mwingine katika eneo hilo anasema, ‘wakati mwengine ndio watu wameteleza na kuanguka lakini wameokolewa, unaona ni nani atakubali kuzunguka mwendo mrefu wenye gharama?ndio maana tunajikuta tukitumia daraja hili ‘.

Maoni yake Werunga ni sawa na ya wengine asilimia karibia 80 ya wakaazi wa eneo hilo ambao wanasema kuwa daraja hili limekuwa kivutio kwa wageni kutokana na muundo wake.

Wanasema kuwa ni daraja la kitamaduni na kwa hivyo hawako tayari kukubali daraja la kisasa kuundwa.

Cha kushangaza ni kuwa licha ya hatari kuu ya daraja hili, kila mtu hulipa ada ya shilingi kumi za Kenya kila wakati kupita.

Na wanaochukua fedha hizi ni wenye mashamba inayopakana na daraja hilo, kila wiki hupokezana fedha makusanyo ya fedha hizo ng’ambo mmoja kwa nyengine .

Facebook Comments